Home » » Mengi yaibuka : Daudi Ballali "Hakuondoka akiwa anaumwa"

Mengi yaibuka : Daudi Ballali "Hakuondoka akiwa anaumwa"

 
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania, Marehemu Daudi Ballali hakuwa mgonjwa wakati akiondoka na aliugua kwa takriban miezi kumi kabla ya kukutwa na mauti, Mei 16, 2008 nyumbani kwake, Washington DC nchini Marekani.



Ballali aliondoka nchini wakati kashfa za wizi kwenye akaunti ya EPA zikiwa zimeshamiri na wakati kesi za watuhumiwa zikianza kusikilizwa huku jina la gavana huyo wa zamani likitajwa, ilitaarifiwa kuwa alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Miezi mitatu baada ya Ballali kuanza kuugua, Rais Jakaya Kikwete alikiri kuwa na taarifa za ugonjwa wake, lakini kakanusha kuwa amekimbia tuhuma za ufisadi zilizokuwa zinaelekezwa Benki Kuu (BoT).

Hata hivyo suala la gavana huyo likaendelea kuwa kitendawili hadi mauti yake, ambayo pia iliamsha mjadala mpya; baadhi wakidai hakuwa amefariki na wengine wakihoji mazingira ya kifo chake.

Lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na baadhi ya ndugu wa marehemu, umebaini kuwa gavana huyo alifariki na kuzikwa nchini Marekani, lakini wakati anaondoka nchini Agosti 2008, Ballali hakuwa mgonjwa kama inavyodaiwa na wengi.

Taarifa kutoka ndani ya BoT alikokuwa akifanya kazi akiwa gavana pia zinasema kiongozi huyo alikwenda Marekani kwa mambo makubwa mawili; Kwanza kufanya baadhi ya kazi zinazohusiana na taasisi hiyo kuu ya fedha nchini na pili kusalimia familia yake ambayo wakati wote imekuwa ikiishi Marekani.

Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu jana alikataa katakata kuzungumza iwapo taasisi yake ina taarifa iwapo Ballali aliondoka nchini akiwa mgonjwa au la, na badala yake akataka suala hilo waulizwe wanafamilia.

“Hayo mambo yalishaandikwa sana na nyie mmeandika sana. Kila mtu anafahamu kwamba aliondoka akiwa mgonjwa, sasa hizo taarifa nyingine unazoniambia mimi siwezi kuzizungumzia. Kaulize familia yake,” alisema Profesa Ndulu.

Wakati Ballali akiwa gavana, Profesa Ndulu alikuwa mmoja wa manaibu wake na baadaye aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya ‘bosi’ wake kuondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kampuni ya Earnst and Young kubaini ufisadi mkubwa kwenye benki hiyo.

Hata hivyo, dada yake na Ballali, Margaret Mpango alisema kaka yake hakuwa mgonjwa na alitarajia kukaa siku chache nchini Marekani.

“Safari yake ilikuwa ya siku chache tu. Alikwenda Marekani lakini alikuwa amepanga kurejea nchini baada ya muda mfupi maana nyumbani kwake simu zake mbili zilikuwa mezani pamoja na funguo za gari ambalo lilikuwa limeegeshwa nje kwa style (mtindo) ambayo ilionyesha kwamba angerudi mapema,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake mjini Kigoma, Margaret ambaye ni mke wa askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Dk Gerard Mpango, alisema baadhi ya nguo za marehemu zilitumwa Marekani baada ya kuanza kuumwa.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency