Home » » Jeshi la Polisi lakamata Dola bandia zenye thamani ya Million 164 Dar.

Jeshi la Polisi lakamata Dola bandia zenye thamani ya Million 164 Dar.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata noti bandia zenye thamani ya Dola 164 milioni za Marekani, sawa na takriban Sh2 bilioni.
Sanjari na hilo, pia limefanikiwa kukamata magari sita, bangi magunia matatu, gongo lita 600 na mitambo sita ya kutengenezea pombe hiyo zikiwamo silaha aina ya SMG, bastola moja, mlipuko mmoja.
Vitu vingine vilivyokamatwa ni magazine mbili za kuwekea risasi, risasi 152 pamoja na watu 18 wanaotuhumiwa kujihusisha na matuko ya unyang’anyi jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema hayo ni matokeo ya operesheni dhidi ya wahalifu iliyofanyika katika wiki mbili kwa mwezi huu na kwamba operesheni hiyo imekuwa na mafaniko makubwa.
Akielezea juu ya washukiwa waliokamatwa na noti bandia, Kova alisema fedha hizo zimekuwa zikitengenezwa na kundi la watu saba ambao walikamatwa maeneo ya Sinza katika Hoteli ya Mombasa wilayani Kinondoni.
Watuhumiwa hao walitajwa kuwa ni Ahmad Mohamed (50) mfanyabiashara mkazi wa Mombasa Kenya, Ichard Magoti (61), mfanyabiashara mkazi wa Musoma, Simoni Lukiko (58), mkazi wa Mogomeni Kagera na Humprey Leonard (34) mlinzi mbaye ni mkazi wa Mburahati Dar es Salaam.
Wengine ni Frank Charles (31) mfanyabiashara mkazi wa Sinza, Abdallah Yusuph (34) mfanyabiashara mkazi wa Sinza na Bakari Bakari (31) mfanyabiashara mkazi wa Mbezi Kimara.
Kamanda Kova alitoa rai kwa wananchi kushirikiana na polisi kutokomeza uhalifu, ili watu waishi kwa amani na kuendesha shughuli zao bila kuhofia uhalifu wa aina yoyote.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova kwa kushirikiana na Kampuni ya Sapna Electronic ametoa simu 20 za mkononi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wa jijini humo ili kuimarisha mawasiliano baina ya polisi na albino wanapopata vitisho.
Kova alichukua uamuzi huo baada ya walemavua hao kutaka kufanya maandamano ya kushinikiza Serikali ichukue hatua stahiki dhidi ya mauaji ya wenzao yanayofanyika nchini hususan mikoani.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency