Home » » Mgogoro wa ardhi Tz:Serikali yabomoa nyumba za wakazi wa Mbezi Beach.

Mgogoro wa ardhi Tz:Serikali yabomoa nyumba za wakazi wa Mbezi Beach.



Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya  Makazi imebomoa nyumba nne zenye thamani ya Sh800 milioni mali ya Tibe K. John zilizojengwa katika eneo la Mbezi Beach bila kibali na kinyume na sheria za mipango miji.

Nyumba hizo zilizokuwa katika Kitalu namba 314 chenye mgogoro wa umiliki, zilikuwa zinajengwa na John kwa kasi bila kujali kuwa kulikuwa na amri ya Baraza la Ardhi ya kuzuia ujenzi huo hadi mgogoro uliohusu eneo hilo utakapotatuliwa.

Wakati wa ubomoaji huo uliosimamiwa na Manispaa ya Kinondoni chini ya Mhandisi Baraka Mkuya, kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi wenye bunduki na mabomu ya machozi, wakiongozwa na Ofisa wa Operesheni, Emmanuel Tille.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Alphayo Kidata alisema kuwa ametoa agizo hilo kwa sababu sheria zinapaswa kuzingatiwa na kwamba nyumba hizo zilijengwa bila kuwa na kibali chochote cha manispaa kama inavyotakiwa.

“Kuwapo kwa kesi mahakamani hakuzuii sheria nyingine kutekelezwa, wamejenga hawana kibali,” alisema Kidata.

Wakili wa John, Emmanuel Augustino alidai kwamba hatua hiyo imetekelezwa kibabe na katibu mkuu, kwa kuwa kuna kesi wamefungua katika Baraza la Ardhi Kinondoni ambayo inaendelea kusikilizwa.

“Anajua wazi kuwa alichokifanya ni kinyume cha sheria, ameingilia uhuru wa mahakama,” alisema.

Augustino alisema hawajui watamshtaki nani ili kudai fidia, hasa kwa kuwa katibu mkuu alitoa agizo la mdomo na hakuna barua yoyote aliyoandika ambayo ingeweza kutumika kama ushahidi.

Wakili wa anayedaiwa kuwa mmiliki wa kiwanja hicho cha Janet Kiwia, ambaye ni Howard Msechu kutoka katika Kampuni ya Uwakili ya Homac, alisema wamefurahishwa na hatua hiyo kwa sababu walikiuka amri ya Baraza la Ardhi ya kupiga marufuku shughuli za ujenzi kuendelea.  

Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency