Home » » Hatimae Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika Desemba mwaka huu.

Hatimae Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika Desemba mwaka huu.




Hatimaye Serikali imetangaza kuwa Desemba 14 itakuwa siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Tangazo hilo lililotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, linasema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yalikuwa yakitegemea matokeo ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

“Katika hatua iliyofikiwa hadi sasa, shughuli za Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hazitaathiriwa na matokeo ya mwisho ya mchakato wa Katiba,” linasema tangazo hilo.

Tangazo hilo limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kuafikiana kuahirishwa kwa Bunge Maalumu Oktoba 4 mwaka huu.

Kwa kujibu wa tangazo lililotolewa, uchaguzi utafanyika katika ngazi za mtaa, kijiji na kitongoji Tanzania Bara kwa ajili ya kuwachagua wenyeviti na wajumbe wa Serikali za vijiji na kamati za mitaa.

Pia, linaeleza kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia masharti ya Sheria za Serikali za Mitaa na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo zimetungwa baada ya kuwashirikisha wadau mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Azaki na wadau mbalimbali.

Ratiba ya uchaguzi inaonyesha kuwa Waziri ataanza kwa kutoa tangazo la uchaguzi, lililoandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa waziri mhusika mwenye dhamana na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Msimamizi wa uchaguzi atatangaza mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji siku 50 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya (6) ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za mitaa, vijiji, vitongoji za mwaka 2014.

Itafuatiwa na wasimamizi wa uchaguzi kuteua majina ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mara baada ya kusambazwa kwa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kisha wasimamizi wa uchaguzi watatoa maelekezo ya uchaguzi siku zisizopungua 28 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 7(1), 8(1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014.

Mwisho, Msimamizi wa Uchaguzi atateua Ofisa wa Umma mwenye sifa na uadilifu ambaye ataandikisha na kuandaa orodha ya wapigakura siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni ya 8 na 9 ya Kanuni za Uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.


Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency