Home » » Hoteli ya Blue Pearl yafungwa kwa sababu ya Deni.

Hoteli ya Blue Pearl yafungwa kwa sababu ya Deni.

Hoteli ya Blue Pearl ya jijini hapa imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa kodi ya pango ya Dola za Marekani 3,800,000 sawa na Sh6 bilioni ambazo alilimbikiza kwa miaka mingi.
Jana mchana wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Majembe walifika hotelini hapo na kuanza kutoa nje samani zilizokuwa ndani ya hoteli na kuzipakia kwenye lori lililokuwa limepaki nje ya lango kuu la kuingilia.


Hali hiyo ilisababisha kusitishwa kwa huduma zilizokuwa zikitolewa na wateja waliambiwa watoke nje kwani hoteli hiyo inafungwa na huduma hazitolewi tena.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Majembe, Seth Motto alisema walifikia hatua hiyo baada ya uongozi wa Hoteli ya Ubungo Plaza ambao ndiyo wamiliki wa jengo hilo kuwaomba wafanye kazi hiyo.
Alisema kazi yao ilikuwa ni kutekeleza ombi hilo la kutoa samani zote zilizokuwa ndani ya hoteli ili mmiliki huyo aweze kulipa deni.
“Tunafanya hivi kwa kufuata utaratibu wa kisheria. Hata kama anasema mkataba wake haujaisha, lakini anatakiwa kufahamu kwamba kitendo cha kushindwa kulipa kodi kimemfanya akasitishiwe mkataba wake…lakini alipewa notice (taarifa) pia. “Wanaendesha hoteli kwa gharama, kwa nini washindwe kulipa kodi,” aliuliza.
Awali, Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Rustan Meran alilalamika kuwa hakupewa taarifa mapema, akisema kitendo kilichofanywa ni kinyume na utaratibu.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alidai kuwa bado wanazungumza nao ili kupata mwafaka wa jambo hilo kwani mkataba wake haujaisha. Alisema mkataba ni wa miaka 15 na imebaki miaka 7 kumaliza.
Naye Mwanasheria wa Majembe, Benard Kuwata alisema wanachofanya ni kuwasaidia Ubungo Plaza walipwe fedha zao.

Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency