Home » » Mfanyakazi MCL apigwa risasi, aporwa Sh2milioni.

Mfanyakazi MCL apigwa risasi, aporwa Sh2milioni.


Watu wasiojulikana wamempiga risasi moja ya mkono na kumpora fedha kiasi cha Sh2milioni mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited, Patrick Pera mara baada ya kutoka kuzichukua katika benki ya NMB tawi la Mandela jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea leo mchana katika kituo cha mafuta cha Oil Com kilichopo katika eneo la Tabata Relini wakati Pera alipokuwa amepakia kwenye pikipiki huku akiwa na idadi hiyo ya fedha kutoka benki
Akizungumza na tovuti hii akiwa katika hospital ya Amana jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa katika hospital ya Taifa ya Muhimbili, Pera ambaye ni Mhariri msaidizi wa habari za kwenye mtandao amesema alifika katika benki hiyo majira ya saa nane ili kuchukua kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matumizi muhimu.
Amesema baada ya kuandikisha fomu na kupatiwa fedha hizo alitoka nje ya benki hiyo na moja kwa moja alielekea kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ili kukodi kwa lengo la kuletwa ofisini kabla ya kwenda kukabidhi fedha hizo kwa kaka yake.
Amesema waendesha bodaboda walianza kutupiana mpira huku kila mmoja akitaka mwenzake ampeleke ndipo kijana mmoja alipoamua kumpakia.
Amesema kabla ya kufika ofisi za MCL wakiwa kwenye kituo cha mafuta cha OIL Com walitokea vijana wengine wawili waliokuwa na pikipiki na kumuamrisha atoe fedha alizokuwa nazo.
Amesema aliwauliza kuwa wao ni wakina nani, ndipo walipomuonyesha bastola na akaamua kuwapatia fedha hizo, lakini kama hiyo haitoshi wakaamua kumpiga risasi moja mkononi.
Tovuti ya mwananchi iliyokuwepo katika hospitali ya amana iliambiwa kuwa risasi iliyopigwa mkononi mwa Pera imesaga mfupa hivyo anahamishiwa kwenye Hospital ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kwa kuwa hospital hiyo haina uwezo wa kufanya hivyo.
Aidha Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi umeanza mara moja kwa kumshikilia na kumuhoji kijana wa Bodaboda aliyekuwa anamuendesha Pera alipokuwa akitokea benki. 
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency