Watu nane wamejeruhiwa, mmoja kati yao vibaya baada ya watu wasiofahamika kurusha bomu katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine uliopo karibu na Mahakama Kuu jijini Arusha.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Issaya Mngulu amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa hakuna aliyepoteza maisha hadi sasa lakini majeruhi mmoja yuko mahututi.
“Hakuna aliyepoteza maisha lakini watu nane wamejeruhiwa na mmoja hali yake ni mbaya, miongoni mwa majeruhi ni watoto wawili wenye umri wa miaka 14 na 15” alisema Kamanda Mngulu.
Kwa mujibu wa Mngulu, madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Selian walikopelekwa majeruhi hao, wamekata mguu mmoja wapo wa majeruhi baada ya kuona umeumia sana.
Hadi sasa hakuna mtu au kikundi kilichotangaza kuhusika na shambulio hilo lakini kamanda Mngulu alisema watu wawili wameshakamatwa wakihusishwa na tukio hilo na kwamba wote ni raia wa Tanzania.
Tukio hilo la bomu katika mgahawa huo ni muendelezo wa matukio ya mabomu yanayoendelea kulikumba jiji la Arusha ambapo mwezi Aprili mwaka huu watu wasiojulikana walirusha bomu katika baa maarufu ya Arusha Night Park na kujeruhi watu kadhaa.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO