Home » » Ndege ya Algerie iliyopoteza rada yaanguka ikiwa na abiria 116

Ndege ya Algerie iliyopoteza rada yaanguka ikiwa na abiria 116


Ndege ya Shirika la Ndege la Algeria (Air Algerie) iliyopoteza mawasiliano ya Rada katika anga la Mali mapema leo ikiwa na abiria 116 na watumishi sita imeanguka, Shirika la Habari la Reuters linaripoti.

Ndege hiyo, AH5017 ilipoteza mawasiliano dakika 50 baada ya kuruka katika Uwanja wa ndege wa Ouagadougou nchini Burkina Fasso na ilitarajiwa kutua katika Uwanja wa Houari Boumediene nchini Algeria saa nne baadaye.

Shirika hilo la habari la Reuters limemkariri afisa mmoja wa Mamlaka ya Anga wa Algeria ambaye hakutaka kutajwa jina lake akithibitisha kuanguka kwa ndege hiyo.

Miongoni mwa abiria waliokuwepo katika ndege hiyo ni raia 51 wa Ufaransa na raia 26 wa Burkina Faso huku maofisa wa Lebanon wakithibitisha kuwepo kwa raia wake wasiopungua 20.

Raia wengine wanaotajwa kuwepo katika ndege hiyo ni kutoka Canada, Ukraine na Luxembourg huku hali mbaya ya hewa ikitajwa kuwa chanzo cha ndege hiyo kupoteza mawasiliano na baadaye kuanguka.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mtandao wa gazeti la The Telegraph, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani ilishatoa onyo juu ya kutumiwa kwa anga la Mali kutokana na kuwepo kwa matukio kadhaa ya waasi.

Kutokana na kupoteza raia wake wengi katika ajali hiyo, maafisa wa usafiri wa anga nchini Ufaransa wamekutana katika kikao cha dharura kushughulikia suala hilo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Waziri Mkuu wa Algeria, Abdelmalek Sellal alisema: “Ndege ilipotea eneo la Gao (Mali) umbali wa kilometa 500 kutoka mpaka wa Algeria, kulikuwa na abiria kutoka mataifa mbalimbali.”

Eneo la Kaskazini mwa Mali limekuwa likikaliwa na waasi wa Kiislamu kwa miezi kadhaa mwaka 2012 na eneo hilo kwa muda mrefu limekuwa katika hali tete kiusalama licha ya waasi hao kusarambatishwa na vikosi vya kimataifa vilivyokuwa vikiongozwa na Ufaransa.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency