Home » » Askofu Kakobe awaunga mkono ukawa

Askofu Kakobe awaunga mkono ukawa




Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe ameongeza chumvi katika Mchakato wa Katiba kwa kueleza kuwa anaunga mkono msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutorejea kwenye awamu ya pili ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.

Kakobe pia alimtupia lawama Rais Jakaya Kikwete akisema  hotuba yake ya kufungua Bunge hilo ndiyo chanzo cha kuvuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.

Kakobe ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita takriban siku tatu tangu Rais Kikwete alipotoa  hotuba yake ya kila mwezi na kujivua lawama hizo alizokuwa akitupiwa na watu wa kada mbalimbali.

“Naunga mkono Ukawa si kwa asilimia 100 bali asilimia 150 kwa msimamo wao wa kususia vikao. Tena sitegemei kusikia wamerejea bungeni, wakirejea watakuwa wamelogwa. Lazima wahakikishe upungufu huo unafanyiwa kazi kabla ya kurejea kwenye awamu ya pili ya vikao hivyo vilivyopangwa kuanza Agosti 5,” alisema.

Aliongeza: “Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo na mapendekezo ya Tume. Sioni kosa langu ni kutoa maoni kuhusu baadhi ya vipengele vya rasimu kwa sababu imetolewa hadharani kwa watu kuijadili. Mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo kama wafanyavyo wengine,” alisema Kikwete kwenye hotuba hiyo.

Hata hivyo, jana Kakobe aliyezungumza kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Kanisa la FGBF alisema kuwa anapingana na utetezi huo kwani hauna hoja ya msingi kwani alishavuruga mchakato huo tangu awali.

“Hotuba yake ya kufungua Bunge hilo ndiyo iliyoharibu mambo yote hadi sasa tumefika katika hali hii.Anafanya hivyo akiwa na dhamira  ya kuvuruga mchakato huo ili usiendelee kwa kuhofia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuanguka katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Mapendekezo ya wananchi,  ambayo yameorodheshwa kwenye rasimu, yanakinzana na matakwa ya chama hicho hiyo ndiyo sababu,” alisema Kakobe kwa msisitizo.

Askofu huyo alisema, ikibidi Rais Kikwete angefanya uungwana kwa kurejea tena kwa wananchi kwa kuandaa hotuba nyingine ili kuwaomba radhi kwa kuvuruga mchakato huo ndiyo mambo mengine yaendelee.

“Hata kama yeye ni kiongozi, kama amekosea, anatakiwa kuomba radhi…lazima awatendee wananchi  haki yao kwa kukiri kuwa yeye ndiye chanzo cha mvurugiko huo ili kuruhusu mchakato wa Katiba uendelee ili Watanzania wapate Katiba wanayoitaka,” alibainisha  Askofu Kakobe na kuongeza:

“Sasa umefika wakati wa chama tawala kukubaliana na mabadiliko yanayotokea. Wananchi wa sasa siyo wale wa zamani wakuburuzwa tu. Siku hizi watu wajanja, watu wanataka kuona maoni waliyopendekeza yanafanyiwa kazi bila kuweka usiasa ndani wala si vinginevyo.”

Alisema kuwa juhudi zote za kuunda kamati  kwa ajili ya kufanya vikao vya maridhiano ili kutaka Ukawa warejee bungeni zimekuwa zikigongwa mwamba kutokana na kukosa uthabiti juu ya hilo.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency