Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amekataliwa katika hoteli moja ya Marekani kwa shinikizo kutoka kwa watu wanaopinga msimamo wake juu ya ushoga nchini mwake.
Hoteli ya Four Seasons iliyopo Irving, Dallas ilitupilia mbali ombi la malazi ya kiongozi huyo kutokana na simu nyingi zilizopigwa na kundi la mashoga kutaka aondolewe hotelini hapo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Dalla Voice, linalodai kutetea haki za mashoga, Rais Museveni alionyesha kukandamiza haki za mashoga Uganda kwa kupitisha sheria inayopinga ushoga nchini mwake.
Hata hivyo, sheria hiyo ilibatilishwa na mahakama kwa kile kilichoelezwa kuwa akidi ya wabunge waliopitisha muswada huo haikutimia kufanya uamuzi huo.
Rais Museveni alitarajiwa kukaa katika hoteli hiyo juzi na jana ambako akiwa Dallas amepangiwa kukutana na Waganda waishio Texas na wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi. Pia, anatarajiwa kuitangaza Uganda kama eneo la kitalii.
Hata hivyo, maofisa wa Rais Museveni walitafuta malazi katika Hoteli nyingine ya Gaylord Texas Resort katika Mji wa Grapevine, umbali wa zaidi ya kilomita 11 kutoka Hoteli ya Four Seasons.
Rais Museveni amekwenda Marekani kuhudhuria kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichoanza Septemba 16 na kitakachokamilika Oktoba Mosi.
Jamii ya mashoga Marekani imepanga maandamano katika maeneo yote atakayotembelea Rais Museveni nchini humo ili kuonyesha kupinga sheria zinazokandamiza haki za mashoga.
Uganda ilianza kutekeleza sheria hiyo dhidi ya ushoga mapema mwaka huu na kufanya ushoga kuwa kosa lenye hukumu hata kifungo cha maisha jela, lakini Agosti mwaka huu kabla ya mkutano wa viongozi wa Afrika na Rais Barack Obama wa Marekani, mahakama ya kikatiba ya Uganda ilibatilisha sheria hiyo.
Hata hivyo hatua hiyo ilitajwa kama isiyotosheleza katika utafutaji wa usawa nchini humo. Juni mwaka huu utawala wa Rais Obama ulifutilia mbali shughuli ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Uganda kupinga sheria hiyo dhidi ya mashoga.
Wizara ya kigeni pia iliweka vikwazo kadhaa vya usafiri dhidi ya maofisa kadhaa wa Uganda walioonekana kukiuka haki za binadamu, wakiwamo mashoga.
Mswada huo awali ulishutumiwa na makundi ya kutetea haki nchini Uganda pamoja na Serikali za Magharibi ikiwemo Marekani kwa sababu ilijumuisha adhabu ya kifo.
Sheria hiyo inatoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa yeyote atakayehukumiwa kwa vitendo vilivyopita mipaka vya ngono kati ya watu wa jinsia moja.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Amama Mbabazi alikaririwa akisema kuwa serikali ya Uganda ingefanya mashauriano zaidi kuhusu mswada huo kabla ya kutiwa saini na Rais Yoweri Museveni kuwa sheria.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO