Sakata la mtoto aliyezamia ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, Karine Godfrey (ambaye sasa imefahamika kwa jina la Happiness Rioba )limechukua sura mpya baada ya mama yake mzazi, Sara Zefhania kujitokeza na kusema kuwa mwanaye hakupanda ndege.
Akizungumza na gazeti hili jana, Zefhania ambaye ni mkazi wa Mkokozi Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani alisema Karine hakupanda ndege ila alipotea.
Alisema mtoto huyo ana tatizo la kutoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha na kwamba hata safari hiyo ilikuwa na utata
Alisema kuwa hata majina aliyotumia siyo majina yake halisi kwani anaitwa Happines Rioba na kwamba hakupanda ndege isipokuwa ni yale mazingira yake ya utata ambayo amekuwa akitumia.
Alifafanua kuwa tabia hiyo ya kutoweka kwa mtoto ilianza mwaka 2010 ambapo alitoweka nyumbani kwa kipindi cha mwezi mmoja na alipatikana mkoani Mwanza akiwa katika mazingira yasiyoeleweka.
Aliongeza kuwa madai ya kusema kuwa alisindikizwa na dada yake kwenda kupanda ndege siyo ya kweli ila ni yeye mwenyewe kutokana na tabia hiyo ya kutoweka na kwenda kusikojulikana.
Alisema mwanaye huyo amekuwa akitoweka nyumbani mara kwa mara kitendo ambacho kinafanya maendeleo ya shule kuwa mabaya na wakati mwingine amekuwa akirudishwa darasa.
Alisema kwa kipindi chote tangu atoweke nyumbani alikuwa akimtafuta sehemu mbalimbali bila ya mafanikio na kwamba jana (juzi) alipata taarifa kuwa mwanaye ameonekana Zanzibar kuwa alionyeshwa katika ITV.
Aliongeza kuwa anapotoweka huwa anatoa taarifa Polisi na kwamba anasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kelezange iliyopo Kitunda na siyo Shule ya Jitihada kama alivyodai mtoto huyo.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO