Home » » Sehemu ya Pili:Mr Chande,Kiongozi mkubwa wa Freemason kutoka Afrika Mashariki akizungumzia yanayowahusu.

Sehemu ya Pili:Mr Chande,Kiongozi mkubwa wa Freemason kutoka Afrika Mashariki akizungumzia yanayowahusu.



Tuhuma za kumwabudu shetani

Kama kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki, Sir Chande alikatishwa tamaa wakati taasisi yake ilipokuwa ikihusishwa na kumwabudu shetani na kutumia nguvu zisizo za kawaida za uchawi kama njia ya kushinikiza uamuzi nchini Kenya.

Mwaka 1994, karibu miaka minane tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Freemason Afrika Mashariki, aliitwa kufika mbele ya Rais Daniel Arap Moi wa Kenya kwenye uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoisakama taasisi hiyo.

“Kwa uelewa wangu, labda siyo kwa mshangao, niliitwa kufika mbele ya tume kwa nafasi yangu kama mkuu, kutoa ushahidi,” anaandika katika kitabu chake.

Ilisemekana kuwa Freemason walikuwa wakiliunga mkono kabila moja lililokuwa likiipinga Serikali na wanachama wake wakimwabudu shetani kwa kusali wakiwa uchi na kutoa kafara za binadamu kwa ajili ya kuchochea nguvu zao.

“Hii haikuwa mara ya kwanza,” anaandika Sir Chande akieleza kwamba pia zimekuwapo kashfa hata kwenye siasa kuhusu Freemason.

“Wachache wanaweza kusahau kashfa ya P2 nchini Italia, ambayo ilileta aibu na kuchafua taswira ya siasa kuhusu Freemason duniani kote,” anaandika.

Sir Chande anasema kuwa, ingawa hakuiona ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza taarifa za Freemason Kenya, taasisi yake haikufanya jambo lolote baya.

“Kwa kuwa tuhuma zilitolewa dhidi ya Freemason Kenya, ziligeuka kuwa baraka, ikatoa nafasi ya kufahamika zaidi katika umma na binafsi, ikizingatiwa kuwa kwenye Freemason siasa ni biashara yako binafsi kama ilivyo dini yako, wala siyo mambo ya majadiliano,” anaandika.

Hata hivyo, Sir Chande anaandika kuwa Tanzania haijawahi kukumbana na changamoto hizo kwenye siasa kutoka serikalini, hata wakati wa Azimio la Arusha kama ilivyotokea Uganda na Visiwa vya Shelisheli.

Kwa mujibu wa Sir Chande, hali hiyo ilitokana na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye wakati wa uhuru aliziangalia taasisi za kujitolea nchini na kuamini kuwa zote zilikuwa zikifanya kazi kwa mrengo wa kusaidia.

Je, Freemason ni taasisi yenye mambo yaliyofichika?

Kwa mujibu wa Sir Chande, Freemason ilianza baada ya Vita ya Pili ya Dunia (WW II), wakati udugu wa Kifreemason walipokuwa wakijaribu kuwalinda wanachama wao waliokuwa Ufaransa, Italia na Ujerumani dhidi ya mateso.

“Tangu wakati huo, tumeingia kwenye jamii na tumekuwa tukipuuza shutuma na kuwaonyesha kuwa taasisi yetu inamchukua mtu mzuri na kujaribu kumfanya kuwa mzuri zaidi, bahati mbaya siyo kila mtu amekuwa akikubaliana na suala hili.Sir Chande anaeleza: “Freemason ni maisha yanayotakiwa mtu ayaishi na siyo kuyafuatilia, ni maisha yaliyojikita kwenye dini, maadili, kulainishwa na ushirika mzuri, kupewa utu kupitia misaada na kujitolea kusaidia.Mafunzo ya Freemason siyo kwa ajili ya leo, bali ni milele. Ni nguvu ya kutenda mema na kuwa imara na inafundisha wanachama wake kuwa imara, kujiheshimu na kuwaheshimu wengine.”
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency