Kamishna wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam SULEMAN KOVA akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam mapema leo
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linakanusha vikali juu ya uvumi unaoendelea jijini Dar es Salaam kuhusu utekaji nyara wa watoto wadogo wanaosoma shule. Hivi karibuni umezuka uvumi kutoka kwa watu mbalimbali hasa wazazi ambao uvumi huu umewafikia kwamba kuna kundi la wahalifu wanaotumia gari aina ya NOAH rangi nyeusi ambao kazi yao ni kuteka nyara wanafunzi kwa nia ya kutenda uhalifu ikiwa ni pamoja na kuwachuna ngozi na madhara mengine.
Mpaka sasa Jeshi la Polisi halina taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara. Pia Jeshi la Polisi limegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo wananchi wanaombwa kuachana na uvumi huo na kuupuuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi.
Aidha, uvumi huu umeanza kuleta usumbufu ambapo mnamo tarehe 03/10/2014 saa tatu asubuhi huko vingunguti mtu mmoja aitwaye PROSPER MAKAME miaka 34, mfanyakazi wa The Guardian Ltd, mkazi wa Tabata akiwa na mkewe MARYSTELLA MUNIS, Miaka 30, mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika maeneo ya shule ya msingi Kombo iliyopo Vingunguti kwa ajili ya kuchukua pesa za vyombo wakiwa na gari aina ya NOAH yenye namba T252 DAY rangi nyeusi.
Ghafla walikuja watu wanaokadiriwa kufikia mia moja (100) na kulizingira gari hilo kwa makelele wakidai kuwa ndilo linalowateka wanafunzi. mtoa taarifa alipoona hali inakuwa tete alipiga simu Polisi na hatimaye watu hao waliokolewa na Polisi kisha kufikishwa katika kituo cha Polisi Buguruni wakiwa salama pamoja na gari lao.
Pia mnamo tarehe 13.10.2014 majira ya saa 10:00 hrs huko katika kituo cha polisi Tabata uliibuka uvumi kuwa gari namba T548 BUN aina ya Noah rangi nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi aitwaye A/INSP ESTAR wa kikosi cha usalama barabarani kituoni hapo ndani yake kuna vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani na kusababisha wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo na wananchi wengine kukusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona hivyo vichwa vitano,na ndipo mkuu wa kituo hicho cha Polisi Tabata aliamuru gari hilo kufunguliwa na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uwongo na uvumi.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linasisitiza kuwa uvumi huu wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu ambao wamekuwa wakiwateka watoto/wanafunzi hao si wa kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo ambazo kwani zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Aidha,uchunguzi wa kubaini ni nani aliyeeneza uvumi huo ulifanyika na kubainika kuwa uvumi na habari hizo zimeenezwa na mtu aitwaye GILBERT s/o STANLEY,(32) mhehe,mkulima,na mkazi wa Tabata ambaye alikamatwa muda mfupi tu baada ya tukio hilo na alipohojiwa alikiri kweli kueneza habari hizo na yeye aliambiwa na mtu mwingine ambaye hata hivyo alisema hamkumbuki.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO