Hii inatisha: Uchunguzi wa DNA wakwamisha kesi ya mauaji.
Uchunguzi wa ushahidi kwa kutumia mashine ya vinasaba (DNA), umekwamisha kesi ya mauaji dhidi ya raia wawili wa Ufaransa kuanza kusikilizwa kwa muda wa miezi tisa kutokana na matokeo yake kutopatikana kwa wakati tangu kutokea kwa mauaji hayo katika Kijiji cha Matemwe, Minazi Mirefu Mkoa wa Kaskazini Unguja Desemba mwaka jana.
Kesi hiyo iliahirishwa mbele ya Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu, Ali Ameir Haji hadi Oktoba 27 na washtakiwa Abdulrahman Thani Matar(39) na Mohamed |Thani Matar(37) wakirudishwa mahabusu kutokana na shtaka hilo kutokuwa na dhamana.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Abdalla Mgongo alimweleza Mrajis wa mahakama hiyo kuwa vielelezo vya kesi hiyo vimepelekwa Tanzania Bara kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia mashine ya vinasaba (DNA), lakini matokeo ya uchunguzi wake bado hayajapatikana.
“Upelelezi wa kesi bado kukamilika, tunasubiri matokeo ya uchunguzi wa ushahidi kwa kutumia mashine ya DNA. Tunaomba kesi kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa,” alisema mwendesha mashtaka huyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Francios Denis Robert na mkewe Brigitte Meny katika Kijiji cha Matemwe Minazi Mirefu, Desemba 2013 kati ya saa 5:50 na saa 7:00 katika Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Kwa mujibu wa sheria namba 7 ya Mwaka 2004 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Zanzibar, ushahidi wa makosa ya kesi ya mauaji, unatakiwa uwe umewasilishwa ndani ya miezi tisa kabla ya mahakama kuchukua uamuzi wa kuifuta kesi au kuwaachia watuhumiwa kwa dhamana.
Inadaiwa kuwa raia hao wa Ufaransa waliuawa na kufukiwa katika kisima, kabla ya kugundulika na mabaki yao kufukuliwa yakiwemo mafuvu mawili ya vichwa, nyonga mbili na viungo vingine vya mikono na miguu.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO