Baadhi ya wafugaji wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wanatumia mbolea ya kupandia na kukuzia mazao kulishia mifugo yao kwa madai kuwa huinenepesha.
Hayo yalielezwa juzi na Ofisa Tarafa ya Makame, Ibrahim Ole Mario alipokuwa akizungumza katika mafunzo ya wenyeviti 25 wa vikundi vya wakulima wa Kiteto, yaliyotolewa na Shirika la Kinapa kwa hisani ya Watu wa Marekani.
Ole Mario alisema matumizi hayo yanaweza kuathiri afya ya ng’ombe na hata ya mlaji, kwani mbolea haikutengenezwa kwa ajili ya matumizi ya chakula cha mifugo bali ni kwa ajili ya mimea.
Alisema njia ya haraka ya kuweza kukomesha matumizi hayo ambayo aliyaita ni ‘haramu’, ni kutowapatia mbolea ya ruzuku wafugaji wote watakaobainika kufanya kitendo hicho.
Alisema huduma ya mbolea itolewe kwa wakulima badala ya kuwapelekea wafugaji ambao wanaitumia kinyume na malengo.
“Hali hii lazima idhibitiwe, haiwezekani tuendelee kuwafumbia macho watu ambao wanabadili matumizi ya pembejeo hiyo, wakati wahitaji wapo na wanakosa huduma,” alisema Ole Mario.
Naye, Mbaruku Chambali alisema tatizo hilo linatokana na matokeo ya Serikali kushindwa kuwafikishia wakulima huduma hiyo tena kwa wakati, hivyo kusababisha waitumie kwa matumizi mengine badala ya yale yaliyokusudiwa.
Alisema elimu duni ya matumizi sahihi ya mbolea ya kupandia na kukuzia mazao, haitolewi ipasavyo, aliwataka maofisa ugani wawajibike katika hilo.
Shirika la Kinapa limekuwa likiwajengea uwezo wakazi mbalimbali wa Kiteto katika nyanja tofautitofauti ikiwamo ya utetezi na ushawishi wa jamii kwa kushirikiana na Watu wa Marekani.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO