Watu 13 wakiwamo wafanyakazi tisa wa Benki ya Stanbic jijini hapa wanashikiliwa na polisi baada ya majambazi kuiba fedha zaidi ya Sh1 bilioni jana jioni.
Watu hao wanashikiliwa katika Kituo cha Oysterbay kwa uchunguzi zaidi wa uporaji huo uliofanywa na majambazi yenye silaha yaliyoingia katika Tawi la benki hiyo la Mayfair Plaza lililopo Barabara ya Mwai Kibaki na kutokomea na kitita hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, aliliambia gazeti hili jana kuwa watu wengine wanne wanaoshiliwa ni askari aliyekuwa lindo na wengine watatu ambao hakuwa tayari kuwataja.
Wambura ndiye aliyeongoza kikosi cha askari kanzu na wenye sare kufanya uchunguzi wa awali katika jengo la benki hiyo ili kujiridhisha na kilichotokea katika tukio hilo. Alisema kiasi kamili cha fedha zilizoibwa kitatolewa baadaye baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao.
“Siwezi kusema leo moja kwa moja kiasi kamili cha fedha zilizoibwa kwa sababu kila mmoja tuliyemhoji anatoa kiwango tofauti,” alisema Wambura.
Hata hivyo, chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kitajwe gazetini, kilidai kuwa hadi jana alasiri, maofisa wa benki hiyo waliokuwa wanashiriki uchunguzi, walibainisha kuwa kiasi cha zaidi ya Sh1.0943 bilioni kilikuwa kimeibwa.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa kiwango hicho cha fedha kinajumuisha sarafu mbalimbali zikiwamo fedha za Tanzania, Euro, Pauni na Dola za Marekani.
Habari zilizopatikana baadaye kutokana katika chanzo chetu, zilidai kuwa fedha zilizoibwa ni Euro 260,000 (Sh598 million), Dola za Marekani 175,000 (Sh280milioni), Sh216 milioni za Tanzania, na pauni 190 za Uingereza (Sh380,000).
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO