Home » » Kutoka Zanzibar : Kijana akamatwa akiwa na mikoba 14 iliyoshehena dawa za kulevya.

Kutoka Zanzibar : Kijana akamatwa akiwa na mikoba 14 iliyoshehena dawa za kulevya.



Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Ali Suleiman Rashid (34) akiwa na mikoba 14 ya wanawake aliyohifadhia dawa za kulevya zenye uzito wa kilo tano akitokea Oman katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume visiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Mkuu ya Polisi Ziwani mjini Zanzibar, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI ), Yussuf Ilembo alisema kuwa mtuhumiwa huyo raia wa Tanzania  amekamatwa muda mfupi baada ya kushuka kutoka Ndege ya Oman yenye namba za usajili .WY.717 iliyokuwa ikitokea Muscat.

Ilembo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 9,  saa 8 mchana akiwa amehifadhi mikoba hiyo katika sanduku kubwa lenye rangi nyeusi na maofisa wa upelelezi waligundua ndani yake kuwemo mikoba 14 iliyokuwa na dawa hizo ikiwa imeshonewa kwa vitu maalumu.

“Dawa hizo  za kulevya zina uzito wa kilo 5.605, zilihifadhiwa kwenye mikoba 14 inayotumiwa na wanawake. Upelelezi kukamilika, atafikishwa mahakamani mara moja,” alisema DCI Ilembo.

Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wake ili kusaka mtandao wa watu wanaojishughulisha na vitendo hivyo kwa kuchunguza njia mbalimbali za mawasiliano za mtuhumiwa huyo aliyekamatwa.

Kwa mujibu wa polisi,  mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia hati ya kusafiria namba AB 363906 iliotolewa Desemba 29 mwaka 2009 Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam na tayari  ameshasafiri katika nchi za Brazil, China, Japan, Hong Kong, Afrika Kusini na Falme za Kiarabu.

Ilembo aliwataka wananchi kuchukua hatua kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwafichua kwa siri, wanaoingiza dawa za kulevya na wauzaji ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

‘Wakati wa kulindana, kuleana na kuoneana aibu umekwisha, kila mmoja ajione ana wajibu wa kulilinda taifa kwa maisha yake na vizazi vijavyo,”alisema DCI Ilembo.

Mapema mwaka huu polisi walikamata mabegi mawili yakiwa na dawa za kuelvya katika chumba cha kuondokea abiria, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency