Home » » Sakata la utupaji wa viungo vya binadamu: IMTU wapanda kizimbani

Sakata la utupaji wa viungo vya binadamu: IMTU wapanda kizimbani

Sakata la kutupwa kwa viungo vya binadamu bila kufuata utaratibu jana liligeuka sinema wakati maofisa wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU), walipofikishwa mahakamani Dar es Salaam.
Maofisa hao ambao ni maprofesa na wahadhiri wa chuo hicho walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kushindwa kufukia viroba 83 vya miili ya binadamu.
Baada ya mashtaka hayo kusomwa na taratibu za dhamana kukamilika huku mmoja wao akishindwa kutimiza masharti, watuhumiwa hao walirejeshwa kizimbani na kufutiwa mashtaka hayo kwa amri ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) aliyewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo.
Hata hivyo, furaha waliyoipata washtakiwa hao, Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar Rao (64), Prabhakar  Rai (69) na Dinesh Kumar (27) ilikuwa ya muda tu, kwani polisi waliokuwapo mahakamani hapo waliwakamata tena na kuondoka nao.
Hati ya mashtaka
Akiwasomea mashtaka, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Polisi, Magoma Mtani alidai kuwa washtakiwa hao Julai 2014 katika eneo la Mpigi Majohe, walishindwa kufukia viroba 83 vya miili ya binadamu waliyoitumia kufundishia wanafunzi wa udaktari kinyume na Kifungu cha 128 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 2002.
Alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kuandaa hati ya ofisa mchunguzi wa vifo vyenye mashtaka (coroner).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo watuhumiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo, Kwey Rusemwa alitoa masharti ya dhamana akiwataka kila mmoja wao kuwa na wadhamini wawili ambao ni raia wa Tanzania na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria.
Washtakiwa watatu walikamilisha masharti hayo lakini mmoja alishindwa kutokana na kuwa na mdhamini ambaye si raia wa Tanzania.
Mashtaka yafutwa
Wakati washtakiwa hao wakikamilisha taratibu za dhamana wakiwa ndani ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali, Salum Ahmed aliingia na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency