Home » » POLISI FFU ADAIWA KUBAKA MTOTO

POLISI FFU ADAIWA KUBAKA MTOTO

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida askari polisi mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Shinyanga anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 13 (Jina limehifadhiwa) na kumsababishia maumivu makali.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama mdogo anayeishi na mwanafunzi huyo polisi huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Alex alitenda kitendo hicho saa nane usiku wa kuamkia juzi huko Ngokolo Manispaa ya Shinyanga baada ya kumkamata kwa nguvu alipokuwa akitokea chooni kujisaidia na kumwingiza chumbani kwake.

Mama huyo alisema mara baada ya kumwingiza chumbani huku akiwa amemziba mdomo kumzuia asipige kelele, alimvua nguo zake za ndani na kuanza kumwingilia kwa nguvu na alipokidhi haja zake alimruhusu kutoka katika chumba hicho na kumtisha kwamba iwapo atamweleza mtu yeyote atamfanyia kitu kibaya ambacho hatakisahau maishani mwake.

“Juzi usiku mnamo saa 8:00 nilisikia mlango ukifunguliwa, nilitoka chumbani kwangu na kwenda kuangalia sebuleni anapolala mwanangu ili kuona ana tatizo gani, sikumkuta sehemu hiyo anayolala, nilihisi ameenda uani kujisaidia na kweli baada ya muda kama robo saa hivi nilimsikia akirudi.”
“Nilitoka na kumuuliza alipokuwa amekwenda akajibu kwa upole alikuwa ameenda kujisaidia, sikumdadisi sana nilirudi chumbani kwangu na nikaendelea kulala, asubuhi kulipopambazuka pia hakuna jambo lolote alilonieleza, nilienda kwenye shughuli zangu na nilirudi nyumbani mchana na kumkuta hayuko katika hali ya kawaida,” alieleza mama huyo.

Alisema hata alipomchunguza alibaini hata kutembea kwake ilikuwa ni kwa shida na ndipo alipomketisha chini kumtaka amweleza kinachomsumbua iwapo anaumwa aseme ili apelekwe hospitali kutibiwa na baada ya kusitasita kwa muda aliamua kueleza ukweli wote kwamba alibakwa na polisi huyo ambaye pia anapanga katika nyumba wanayoishi.

“Kwa kweli aliponipa taarifa hiyo nilisikitika sana, nilichukua hatua ya kumsubiri huyo polisi atoke kazini ambapo nilimuuliza kwa nini alimfanyia mwanangu kitendo kiovu, mwanzo alisita kukubali, lakini baadae alikiri na kusema alikuwa amepitiwa na kujikuta akimfanyia kitendo hicho.”
“Hata hivyo alinishangaza baada ya kunihoji kwamba baada ya kufanya hivyo mimi nataka nini, sikuridhishwa na majibu yake, nilitoka na kwenda kumwalifu mchungaji wa kanisa letu ili aweze kunisaidia juu ya hatua za kumchukulia polisi huyo, alipokuja aliamua pia tuwaarifu watu wa Agape ili waweze kutusaidia kupata msaada wa kisheria,” alieleza.

Mama huyo alisema baada ya kuwasiliana na watu wa Shirika la Agape waliongozana pamoja na mtoto aliyebakwa hadi katika kituo cha polisi ambako walipewa fomu namba tatu kwa ajili ya kwenda hospitali kupimwa na baadaye walirejea kituoni na mtoto huyo alimtambua mtu aliyembaka na kutoa maelezo katika dawati la jinsia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba atatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi ambao tayari unaendelea kufanyika.

Chanzo: Majira
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency