Home » , » MAYAI YA KWARE SASA NI KIKOMBE CHA LOLIONDO

MAYAI YA KWARE SASA NI KIKOMBE CHA LOLIONDO


Hivi sasa kumeibuka tiba ya ‘mayai ya kwale’ ambayo inavuma kila kona na imekuwa gumzo kila mahali. Tiba hii ni ya kimaajabu kwani uvumi uliopo ni kwamba mayai ya kwale yana uwezo wa kutibu magonjwa yote sugu.
Kasi ya kushauri wagonjwa na hata wasio wagonjwa kutumia mayai haya badala ya kwenda hospitali kwa uchunguzi wa afya zao inaongezeka na maelekezo yanayopatikana mitaani juu ya kutumia tiba hii ni ya ajabu na yanatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Nilishuhudia mtu mmoja akimwelekeza mgonjwa kuwa alipaswa kuyapasua mayai na kuyapondaponda pamoja na magamba yake na kisha ayanywe katika hali ya ubichi. Mwingine aliambiwa ayapasue na kisha ayakoroge pamoja na asali au maziwa kisha anywe, wengine wanaelekezwa kuyachemsha kama mayai ya kawaida na kisha kula kiini cha ndani. Uvumi huu unaenea kwa kasi mitaani.
Kutokana na kuvuma kwa tiba hii, mayai haya hivi sasa yanaonekana kusakwa kila mahali na yanauzwa kati ya Sh15,000 hadi 20,000 kwa trei.
Uvumi wa tiba hii hauna tofauti na ule uliozuka nchini juu tiba maarufu kama ‘kikombe cha Babu’. Watu wengi walikatisha matibabu kwenye hospitali mbalimbali na kuamua kwenda Kijiji cha Samunge kwenda kupata kikombe cha babu na kufanya kuwe na misururu mirefu ya watu waliokesha usiku na mchana. Hii ilizusha adha kubwa hasa kutokana na kutokuwepo na maandalizi ya vyoo hivyo watu kujisaidia ovyo vichakani.
Adha ya safari ndefu na kukaa kwenye foleni kwa zaidi ya siku tatu, kulifanya wenye afya mbaya kushindwa kuhimili na hata kupoteza maisha.
Katika mazingira haya ya kuibuka tiba za ajabuajabu ambazo hazijathibitishwa kitaalamu, ni vyema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikatoa ufafanuzi.
Isisubiri hadi watu wapoteze maisha halafu ndiyo ianze kuja na maelekezo tena yanayopingana na yale ambayo jamii inaamini. Kuchelewa kunafanya wengi wapoteze fedha na hata kuacha tiba sahihi na kukimbilia kitu ambacho kinavumishwa tu.
Serikali haipaswi kukaa kimya wakati watu wakiendelea kutibiana kwa vitu ambavyo havijathibitishwa kitaalamu.Kama Serikali ingechukua hatua mapema, watu wasingepoteza maisha kupitia kikombe cha babu.
Uvumi huu wa tiba ya mayai ya kwale hauna tofauti na Kikombe cha Babu.
Katika ulimwengu huu wa utandawazi na soko huria, ni kawaida kusikia mambo mapya yakiibuka kila kukicha, lakini kama mambo hayo yanagusa afya zetu, hatuna budi kuwa makini na waangalifu zaidi.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency