Part 2:Mapya mazito yaibuka Baada ya Nyalandu kufanyia kazi video ya Msigwa.
Kampuni ya Green Mile Safari Limited (GMS) iliyofutiwa leseni ya uwindaji wa kitaliii na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu Julai 11, imeziomba mamlaka za juu kuingilia kati uamuzi huo kwa madai ya kutotendewa haki.
Mwanasheria wa GMS, Alloyce Komba alisema jana kuwa wanatarajia Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda watafuatilia suala hilo kwa karibu na kutumia utawala wa sheria kutoa haki stahiki kwa kuwa Nyalandu hakuwapa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.
GMS ilifutiwa leseni na kunyang’anywa vitalu vyake eneo tengefu la Ziwa Natron Mashariki, Gonabias/Kidunda WMA na kile cha pori la akiba la Selous MK 1 kwa madai ya kufanya makosa ya kuwinda wanyama jike na wadogo, kumruhusu mtu wa chini ya miaka 18 kuwinda, kuwinda na kuwanyanyasa wanyama kupita na gari ndani ya eneo la kuwindia kinyume na Sheria Namba 5 ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009.
Hatua hiyo ya Nyalandu ilikuja baada ya waziri kivuli wa Maliasili na Utalii, Peter Msigwa kuzungumza bungeni juu ya tuhuma hizo na baadaye kuonyesha waandishi video ambayo alisema inayoonyesha wateja wa GMS wakiwinda kiharamu, ikiwamo kutumia bunduki kali zilizowekewa viwambo vya sauti.
Komba alisema hatua ya kufungiwa leseni hizo imeibuka baada ya kuwapo kwa mgogogro wa kitalu tengefu cha Ziwa Natron Mashariki na mmiliki wa awali kampuni ya Wengert Windorse Safaris Limited (WWS) ambayo ni kampuni tanzu ya Friedlkin Conservation Fund ya Marekani.
Kwa mujibu wa Komba, WWS walikosa sifa ya kumiliki kitalu hicho na baadaye walianza fitna zilizopelekwa hadi Ikulu ya Marekani kwamba Wizara ya Maliasili imewanyang’anya kitalu chao.
Komba pia alimtuhumu Msigwa kutumika na Nyalandu ili kufanikisha mchakato wa kampuni hiyo kunyang’anywa vitalu jambo ambalo waziri huyo kivuli alilikana. Msigwa alisema aliipata video hiyo wiki moja kabla ya kuwasilisha hoja yake bungeni na kwamba iwapo angeipata mapema basi angechukua hatua stahiki.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO