Aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe pamoja na aliyekuwa naibu wake anayeshughulikia huduma, Hamad Mussa Koshuma wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la matumizi mabaya ya madaraka.
Mgawe na Koshuma walifikishwa mahakamani hapo na mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincoln jana asubuhi na baadaye Wakili Mkuu wa Serikali (PSA), Oswald Tibabyekomya aliwasomea shtaka.
Katika shtaka hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa nafasi zao kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa bandari kwa Kampuni ya China Communications Company Ltd ya China, bila kutangaza zabuni hiyo.
Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Tibabyekomya alisema kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Desemba 5, 2011 wakiwa Mamlaka ya Bandari Tanzania, jijini Dar es Salaam, wakati wakitekeleza majukumu yao ya utumishi wa mamlaka hiyo kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu na naibu wake.
Alisema kuwa washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka ya kuingia mkataba wa kibiashara kati ya TPA na Kampuni ya China Communications Company Ltd, kwa ajili ya ujenzi wa ghati namba 13 na namba 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakili Tibabyekomya alifafanua kuwa washtakiwa hao waliingia mkataba na kampuni hiyo bila kutangaza zabuni hiyo, kinyume cha masharti ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, namba 21 ya mwaka 2004, kwa lengo la kuinufaisha kampuni hiyo.
Hata hivyo washtakiwa hao walikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa. Wakili wa washtakiwa hao, Samson Mbamba aliomba mahakama iwape dhamana wateja wake kwa kuwa shtaka lao linalowakabili linadhaminika, na Hakimu Isaya Alfani aliweka wazi dhamana hiyo, akiweka sharti la dhamana ya Sh2 milioni.
Sharti jingine la dhamana ni kila mshatakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuamini ambao pia watasaini dhamana ya Sh2 milioni.
Washtakiwa wote walitimiza masharti hayo na kuachiwa huru kwa dhamana hadi Agosti 13, 2014, kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Kabla ya kupandishwa kizimbani jana, Mgawe, Koshuma na vigogo wengine watatu walisimamishwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, na baadaye kuwafukuza kazi kabisa kutokana na tuhuma mbalimbali.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO