Majambazi wamevania na kupora Sh17 milioni katika Baa ya Break Point iliyopo eneo la Makumbusho Kijitonyama, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana wakati mmiliki wa baa hiyo, Daudi Machumu alipopeleka fedha hizo kwa meneja wake ili aweze kufanya malipo kwa mawakala wake wa vinywaji.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema watu hao hao walifanikiwa kukimbia baada ya kuiba kiasi hicho cha fedha na hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Wambura alisisitiza umuhimu wa kufanya malipo kwa njia ya benki ili kuepusha athari ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara na kugharimu maisha ya watu na upotevu mkubwa wa fedha.
“Kila siku tunawaambia watu wasifanye malipo kwa fedha taslimu lakini hawasikii. Watambue kuwa majambazi nao wanatafuta upenyo wa kufanya uporaji,” alisisitiza kamanda huyo na kusema polisi haiwezi kulinda mifuko yao.
Alisema huo ni uzembe wa mmiliki wa baa hiyo kwani kila siku wanasisitiziwa juu ya kufanya malipo kwa njia mbadala.
Huu ni mwendelezo wa matukio ya ujambazi nchini ambayo yamekuwa yakihusisha uporaji wa fedha nyingi sambamba na mauaji ya watu wanaokuwa na fedha hizo mkononi.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO