Jeshi la Polisi mkoani Arusha, limezima maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana baada ya askari wake wa miguu na magari ya maji ya kuwasha kutanda mitaani, huku chama hicho kikidai kufanikiwa kufikisha ujumbe uliokusudiwa.
Idadi kubwa ya polisi ilitanda maeneo ambayo maandamano hayo yalitarajiwa kupita, kuanzia eneo la Philips na Usa, Wilaya ya Arumeru na katika vituo vya polisi.
Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari waliotangazwa kuongoza maandamano hayo walikuwa chini ya ulinzi mkali.
Nassari alisema alishtushwa na magari manne yenye askari kuegesha nje ya nyumba yake tangu asubuhi sanjari na kutapakaa mitaani.
“Mimi naishi njia ya Momera Kijiji cha Ngurdoto. Tangu asubuhi polisi wamezingira nyumba yangu nikaona ili kutosababisha maafa nisitoke,” alisema.
Kwa upande wake Lema pia alikuwa katika ulinzi na kwamba licha ya kufika eneo la Philips, alishindwa kuanzisha maandamano baada ya polisi kulidhibiti eneo hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema kuwa kusambaa polisi mitaani kumefikisha ujumbe wao wa kupinga Bunge la Katiba kuendelea.
“Hii ni mbinu mpya, hatukutaka ujumbe kubadilika kuwa Arusha mabomu tena. Tumefanikiwa kusambaza ujumbe mitaani. Mfumo huo, tumeupa jina la ‘Non Violence Demonstration’(NVD) na utaendelea kwa wiki nzima,”alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kueleza waliokamatwa baada ya simu yake kutopokewa.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO