Hakuna marefu yasiyo kuwa na ncha, ni usemi wa zamani wa wahenga wenye maana ya kila jambo lenye mwanzo, lazima litakuwa na mwisho.
Ndivyo ilivyo kwa Bunge la Katiba ambalo safari yake ilianzia Februari 18 mwaka huu na kutarajia kuhitimishwa Oktoba 4 kwa ajili ya kutoa Katiba inayopendekezwa.
Yapo mengi yaliyofanyika ndani ya Bunge hilo yakiwamo mazuri yaliyofurahisha masikioni mwa watu, licha ya kuwa kuna baadhi ya mambo yaliyotoa tafsiri hasi kwa makundi yote.
Mbali ya hayo, ziko ndimi ambazo zilipasua Bunge hilo na hata wakati mwingine kusababisha mivutano mikali kiasi cha kuleta mkanganyiko uliotafsiriwa kivingine.
Kikubwa ni kuwa, sasa mchakato huo unafikia mwisho ili ipatikane Katiba inayopendekezwa ambayo itawekwa kabatini ikisubiri rais ajaye ambaye ataanzia kura ya maoni kwa wananchi baada ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Mjadala wa Bunge hilo ulitikiswa na mengi lakini kumi ndiyo hasa yalionekana wazi kuleta mvutano mkali kiasi cha kuligawa Bunge hilo ikiwamo suala la kura ya wazi au kura ya siri.
Jambo hilo liliibuka katika hatua ya awali ya kutunga Kanuni zitakazoongoza Bunge hilo. Hofu ya wajumbe ilikuwa kama kura zingepigwa kwa wazi, kungeibuka hofu kutoka kwa baadhi ya wajumbe ambao wangeogopa kusurubiwa na vyama vyao au makundi waliyotoka kushughulikia kama wataenda kinyume na matakwa ya vyama au makundi hayo.
Hata hivyo hali ilikuwa kinyume katika hitimisho, baada ya wajumbe hao waliokuwa wakitaka kura ya siri kugeuka na kupiga kura ya wazi licha ya kuwa uhuru ulitolewa wa aina mbili za kura.
Jambo la pili lililochomoza ni suala la uraia pacha. Hapa palichimbika. wajumbe wote walionyesha umahiri wa kuzungumza na kujenga hoja wakitaka kuungwa mkono. Kadari Singo ni Mjumbe aliyeingia katika Bunge hilo akiwakilisha kundi la watu wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), alisimama kidete kulilia haki ya urais pacha ambayo ilionekana kuwagusa watu wengine ambao walikuwa wakimuunga mkono, huku hoja mbalimbali zikijengwa kwa ajili ya kutetea jambo hilo.
Lakini mwishowe suala hilo lilipingwa kwa sehemu kubwa na watawala ambao wamelijengea shaka licha ya kuwa baadhi yao ndiyo wenye ndugu na watoto walio nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, hekima ya Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sitta ilitumika kuzima suala la Mahakama ya Kadhi ambalo liliibuliwa na watu wa imani ya Kiislamu.
Mbunge aliyewasha moto huo alikuwa Mtutura Abdalah Mtutura ambaye katika mchango wake aliwahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kutokuunga mkono Katiba kama haitakuwa na sura ya Mahakama ya Kadhi. Nalo liliishia kwa mbunge huyo kuomba msamaha na Sitta kulisawazisha kwa kutoa ahadi ya kuliweka katika mfumo mzuri ndani ya Katiba.
ambo la nne lililotikisa ni wajumbe wenye mamlaka kupinga Rasimu ya Katiba katika kipengele cha wabunge kuwa mawaziri. Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka walipinga hoja hiyo.
Viongozi hao walizungumza kwa mifano namna inavyokuwa ngumu kwa waziri ambaye ni mbunge kutekeleza majukumu yake. Wanasema anakosa muda wa kuwatumikia wapiga kura wake kikamilifu.
Mjadala huo pia ulikolezwa na suala la kiwango cha elimu kwa mbunge. Licha ya Tanzania kuwa na utitiri wa shule za Sekondari, mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde, aliongoza hoja ya kutaka sifa ya kugombea nafasi za kisiasa ibaki kuwa ni kujua kusoma na kuandika.
Ilikuwa kama masihara lakini mwakilishi huyo alijenga hoja ambayo ilionekana kuungwa mkono na watu wengi huku wengine wakipinga. Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge ni miongoni mwa wajumbe waliopinga hoja hiyo.
Suala la muungano nalo lilivuta hisia kali hasa katika kipengele cha nafasi ya Rais, Makamu na Waziri Mkuu. Hapa wajumabe walijikuta wakikwepa mvua na kukanyaga umande. Rasimu ilipendekeza Serikali tatu ambazo zingekuwa na marais watatu, lakini wao wakapigia chapuo Serikali mbili zenye rais wawili na Makamu watatu.
Pendekezo la walio wengi ni kuwepo kwa rais wa Muungano, Makamu wake, rais wa Zanzibar kuwa Makamu na Waziri Mkuu kuwa katika nafasi ya umakamu pia kama ilivyo mwanzo kabla ya mfumo wa vyama vingi. Wanawake kwa upande wao walionekana kujipanga zaidi katika usawa wa kijinsia kwenye uongozi kutoka ngazi ya chini hadi juu. Jambo hilo lilileta msuguano wa uelewa lakini mwisho lilihitimishwa kwa wengi kulikubali.
Pia kulikuwa na hoja ya wabunge kuwajibishwa na wananchi pale wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo. Hapa Bunge liligawanyika kati ya wajumbe wa kundi la 201 na wale ambao wanatoka katika Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi.
Kundi la 201 walitaka kipengele hicho kibaki wakati wengine wakitaka kiondolewe kabisa.
Hoja nyingine ikawa ni suala la mfuko wa pamoja na hadhi ya Zanzibar katika masuala mazima ya fedha ikiwamo kilio cha kutaka mgao wa fedha za misaada ziongezwe katika upande huo wa pili wa Muungano badala ya kile cha sasa cha asilimia 4.5.
Pamoja na wote kujitahidi kuliweka sawa jambo hilo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini Alli Keissy Mohamed alitibua mambo, baada ya kueleza kuwa Wazanzibari hawana kitu na kwamba wanaishi kwa fadhila za Tanganyika.
Nusura ngumi zipigwe ndani ya ukumbi wa Bunge hilo na kama si watu wa usalama kusimama kidete, huenda mambo yangeharibika, kwani kila mmoja alionyesha kuchukizwa na maneno ya mbunge huyo ambaye tangu wakati huo hadi sasa anasimamia msimamo wa Serikali tatu ili kuwepo na hali ya kila mmoja kuwajibika.
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO