
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo amezindua kampeni ya usafi ya mkoa iliyofanyika katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Kampeni ya usafi ya siku 90 inayobeba kauli mbiu “usijifanye mstaarabu kuwa mstaarabu” itaanza kesho (1/5/2016) kwa lengo la kuboresha hali ya usafi katika mitaa mbalimbali pamoja na jiji la Dar es salaam kwa ujumla, ambapo itasaidia kuzuia magonjwa ya mlipuko, na wakazi wa jiji hilo wamehamasishwa kushiriki kufanya usafi katika mitaa yao pamoja na maeneo mbalimbali na baadae washindi kupatiwa zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni 100 kwa mitaa miwili itakayokuwa imeshinda, ambapo pia Mkuu huyo wa mkoa aligawa vifaa vya usafi kwa wenyeviti wa mitaa kutoka wilaya zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke.
Bw. Makonda amesema kuanzia sasa wakazi wa jiji la Dar es salaam watafanya usafi katika mitaa na maeneo yao kila siku ya jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi, na baada ya siku 90 washindi wawili, ambapo mtaa utakaokuwa msafi na wenye makazi yaliyo katika mpangilio mzuri utapata zawadi ya fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 50 na mtaa utakaokuwa msafi lakini hauna makazi yaliyo katika mpangilio mzuri nao utapata fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 50, vilevile mtaa utakaoongoza kwa uchafu utatangazwa ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wake kueleza namna ambavyo ameshindwa kusimamia usafi katika eneo lake.
Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi wakiwa na Naseeb Abdul “Diamond Platnumz ” Simba, Babu Tale, Ruge Mutahaba wa Clouds Fm na wengine wengi wakishiriki Kampeni ya Usafi Leo Dar ya Makonda. (Picha na Othman Michuzi wa Mtaa kwa Mtaa Blog)
“Mganga Mkuu wa Mkoa atafanya ukaguzi na kutangaza vigezo vya washindi baada ya siku 90, tangu kuanza kwa kampeni hii, tunataka kuona mabadiliko na watu lazima washiriki kwa usafi na kuyapaka rangi majengo yao. Suala la usafi si la Serikali pekee ni letu sote” alisema Makonda.
Aidha, ameagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri kwa Mkoa wa Dar es Salaam hasa daladala kuwa na vifaa vya kutupia taka katika vyombo vyao na kuanzia mei 2, atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa kampuni, taasisi na watu mbalimbali kuunga mkono zoezi hilo kwa kutoa misaada mbalimbali ikiemo kuhamasisha wananchi juu ya suala hili. Pia amewapongeza wakazi wa mkoa huo kwa kushiriki kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni ya usafi na kuzipongeza kampuni za Clouds Media group, Azam na redio ya EFM kwa michango yao katika kufanikisha kampeni hiyo ya usafi kwa mkoa wa Dar es salaam.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi, amewasisitiza wakazi wa mkoa wa Dar es salaam kufanya zoezi la usafi kuwa endelevu kwa kuwa wananchi wenyewe ndio wazalishaji wakubwa wa uchafu hivyo ni lazima wahahikishe wanauondoa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh.Paul Makonda (wa pili kushoto),akiwa sambamba na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa za Wilaya ya Kinondoni,Ilala pamoja na Temeke wakishiriki kwa pamoja kufagia ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono Mh Paul Makonda kuzindua kampeni ya Usafi wa jiji la Dar Es Salaam,uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika mapema leo asubuhi Katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali serikali,dini na makundi mengine yakiwemo makundi ya michezo na waendesha boda boda.Mkuu wa Mkoa alizindua kampeni hiyo ya Usafi kwa kuwakabidhi Wenyeviti hao kila mmoja ufagio wa ajili ya kwenda kuwahamasisha wananchi wao katika mitaa yao.
Naye, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria Bw. Mustafa Mkama, amesema wanafunzi wa vyuo mbalimbali wanaunga mkono kampeni hii na kuitaka jamii kwa ujumla ibadilike kwa kufanya usafi na Serikali nayo ihakikishe inaweka vyombo vya kuhifadhia taka katika maeneo mbalimbali, sambamba na kuendelea kuelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na mazingira safi.
Uzinduzi wa kampeni ya usafi ya mkoa wa Dar es Salaam ulitanguliwa na maandamano ya Mkuu wa Mkoa, viongozi mbalimbali wa dini na vyama vya siasa, wasanii mbalimbali akiwemo msanii wa muziki wa kizazi kipya Nasibu Abdul maarufu kama Diamond platnamz pamoja na wakazi wa mkoa huo, ambayo yalianza katika wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni na kuishia katika viwanja vya Leaders.
Ikumbukwe kuwa 9 desemba 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alihairisha shamrashamra za sherehe za Muungano na kufanya usafi, huku akiwataka watanzania wote kushiki kufanya usafi katika maeneo yao na kuagiza kuwa zoezi la kufanya usafi kuwa endelevu nchi nzima.
Angalizo
Naomba vijana wote watakokuwa tayari kushiriki kufanya usafi katika sehemu mbalimbali za jiji letu ,tuwasiliane kupitia:
Simu namba : 0625934656
Barua Pepe : hassanmohamedtoziri@gmail.com
0 comments:
BONYEZA HAPA KUACHA MAONI YAKO