Home » » Bunge la Katiba ngoma nzito

Bunge la Katiba ngoma nzito


Dodoma. Hofu imetanda kuhusu uwezekano wa kuvunjika kwa Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na hatua ya CCM kutumia wingi wao kutaka kupitisha utaratibu wa kupiga kura za wazi.

Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wameshauri njia pekee ya kunusuru mchakato huo ni kwa CCM kukubali kukaa meza ya mazungumzo.

Wakati wajumbe hao wakitoa angalizo hilo, taarifa zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema CCM, wameitisha kikao cha dharura cha wajumbe wake wote leo saa 8:00 mchana kwa agenda ambayo bado ni siri.

Habari hizo zinadai kuwa wajumbe ambao ni Wabunge na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wametumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) wakitakiwa kuhudhuria kikao hicho bila kukosa.

“Mambo muhimu yatajadiliwa, Mwenyekiti wa Cocas (umoja wa wabunge) anasisitiza mhudhurie bila kukosa, mahudhurio yatazingatiwa,” unasomeka ujumbe huo ambao gazeti hili limeuona.

Baadhi ya wabunge wa CCM hususan wanaotoka Kanda ya Ziwa wanaounga mkono kura ya siri, walidai kuwa kikao hicho huenda kina nia ya kuwatisha ili walegeze msimamo wao.

“CCM wanaogopa kura za siri kwa sababu moja tu, wakiiruhusu watakuwa hawana control (udhibiti) wa wajumbe kutoka Zanzibar ambao wengi wanataka Serikali tatu,” alidokeza mbunge mmoja ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe.

Mbunge huyo alisema kwa tathmini yake, kama utaratibu wa kura za siri utapita, karibu asilimia 80 ya wajumbe wote kutoka Zanzibar, watapiga kura ya kupitisha rasimu ya muundo wa Serikali tatu.

“Kwa hiyo CCM haitaki kabisa utaratibu wa kura za siri, wanataka kura za wazi ama kura ya dhahiri ili waweze kuwa na udhibiti wa wajumbe ili tusitoke nje ya msimamo wao,” alidai mbunge huyo.

Hata hivyo, wakati CCM ikishikilia msimamo wa kura za wazi katika kupitisha rasimu hiyo, wabunge wake wengi wa Tanzania Bara na wale wa Zanzibar wanataka upigaji wa kura za siri.

Akizungumza na gazeti hili jana, James Mbatia alitahadharisha kuwa msimamo wa CCM kulazimisha kura za wazi, siyo kuwatendea haki Watanzania na huenda ikawa chanzo cha machafuko na kukwama kupatikana Katiba Mpya.

“Kulazimisha matakwa ya CCM badala ya wananchi itakuwa ni chanzo cha machafuko na Watanzania hatuko tayari kwa machafuko wala kuona damu ya Mtanzania inamwagika,” alisema Mbatia.

Chapisho: Gazeti la Mwananchi
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency