Home » » Watu 20 wauwawa Kenya katika shambulizi la jana usiku

Watu 20 wauwawa Kenya katika shambulizi la jana usiku



TAKRIBAN watu 20 wameuawa katika shambulizi la pili la usiku katika pwani ya Kenya.
Kundi la wapiganaji la Al Shabaab limekiri kutekeleza shambulizi hilo la pili katika vijiji viwili zaidi na kusema wengi waliouawa ni maafisa wa polisi.
Wapiganaji hao walivamia vijiji viwili karibu na mji wa Mpeketoni, ambao ni eneo la mashambulizi ya kwanza yaliyosababisha mauaji ya watu 48.
Tukio hilo limetokea licha ya maafisa wengi wa polisi kupelekwa katika eneo hilo kufuatia mauaji hayo ya Jumapili.
Kwa mujibu wa BBC, wakazi wa eneo hilo wamelalamikia Serikali kwa kutowapa ulinzi baada ya shambulizi la kwanza na sasa wanaishi kwa hofu.
Serikali imesema wanamgambo wa Al Shabaab walikata mawasiliano ya simu katika eneo hilo kabla ya kutekeleza shambulizi hilo.
Wanamgambo hao wanaohusishwa na kundi la Al Qaeda wamesema wataendelea kufanya mashambulizi nchini Kenya ikiwa serikali haitaondoa wanajeshi wake nchini Somalia.
Shambulizi hilo la vijijini limeonekana kuwa mfumo mpya wa mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Al Shabaab ambao mara nyingi wamekuwa wakilenga maeneo ya mijini hasa miji mikubwa.
Takriban watu 48 waliuawa katika mashambulizi yaliyofanyika usiku wa kuamkia Jumatatu huku watu wenye silaha wakishambulia hoteli na kituo cha polisi pamoja na kuteketeza magari.
Wakati huohuo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema mauaji yaliyofanywa katika mji wa Mpeketoni hayakufanywa na kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Al Shabaab.
Kauli ya Rais Kenyatta inakuja kupitia televisheni siku moja baada ya kundi hilo kukiri kufanya mauaji yaliyotokea Mpeketoni Jumapili usiku.
Rais Kenyatta amesema kuna ushahidi kuonesha kuwa shambulizi hilo lilipangwa vyema na kwamba wanasiasa nao walihusika.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency