Home » » Baraza la maaskofu latoa tamko juu ya Bunge la Katiba.

Baraza la maaskofu latoa tamko juu ya Bunge la Katiba.





BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa waraka wa pili kuhusu Katiba mpya kwa Watanzania, ambao umetuma ujumbe mzito kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ukisisitiza Katiba ijayo iwe ya kuleta mema, kuimarisha amani na utulivu wa nchi.

Akitoa tamko hilo mjini Iringa jana, Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema ikiwa matokeo yatakuwa yenye kuleta mema hayo, Watanzania wote watawashukuru na kuwasifu wajumbe hao.

Hata hivyo, Askofu Ngalalekumtwa alionya kuwa kama tunda la kazi ya Bunge hilo, itakuwa lenye kuingiza nchi katika matatizo zaidi na kuwataabisha wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi Watanzania watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika jukumu hilo muhimu walilokabidhiwa.

Waraka kwa kwanza

“Katika ujumbe wetu wa Kichungaji wa Pasaka 2014 (Waraka wa kwanza), sisi maaskofu Katoliki Tanzania tuliwaandikia barua watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu, tukiwaalika kuchukulia maanani mchakato wa kuandika Katiba mpya. “Wakati huu (waraka wa pili), tunawaalika Watanzania wote kwa pamoja, tuungane kuwakumbusha wale waliopewa dhamana ya kukamilisha Katiba itakayopendekezwa, kuwajibika binafsi na katika maridhiano kutupatia Katiba maridhawa,” alisema.

Alisema wajumbe wa Bunge hilo, wanapaswa kujadili kwa umakini kila kilichopo katika rasimu hiyo ya Katiba, ili wafikie muafaka utakaoenzi ujasiri wa kipekee wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wa kuanzisha mchakato huo.

“Tunawaasa tukiwaombea dhamiri zao zipate maoni mapya, ili wabebe kikamilifu dhamana hiyo waliyokabidhiwa,” alisema.

Sifa za Katiba

Askofu Ngalalekumtwa alisema nchi haiko tayari kurudi nyuma na kuendelea na maisha yanayoongozwa na Katiba ya 1977, kwa hiyo mahitaji ni kuwa na Katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika uamuzi na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Alifafanua kuwa kadri nchi ilivyo hivi sasa, kuna sababu za kutosha za kutaka Katiba mpya, ikiwa ni pamoja na ufisadi, wananchi kujisikia kukosa usalama na amani, nchi kutokuwa na dira na tunu za msingi.

“Tunataka Katiba ambayo inaruhusu utawala wa sheria, haki sawa kwa wote, manufaa na ustawi kwa wote na kuheshimu utu wa kila mmoja. Katiba shirikishi katika matumizi ya madaraka, ili yatumike katika kuhudumia wote badala ya wachache na inayoweza kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi,” alisema.

Misimamo vya vyama

Kuhusu misimamo ya vyama vya siasa, Askofu Ngalalekumtwa alianza kwa kuweka wazi kuwa, “Baraza la Maaskofu Katoliki halina chama katika hili, lakini pia halina mtu au mwanasiasa au chama linachokifanyia kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.”

Hata hivyo, kwa kutambua uwepo wa wanasiasa katika Bunge hilo, ambao walitumia misimamo vya vyama vyao zaidi katika Bunge lililopita, Askofu Ngalalekumtwa alisema TEC inawataka wajumbe wa Bunge hilo kuwa wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama.

“Kuandika Katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama, na hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda Katiba mpya kwa kuzingatia Rasimu ya Pili utaweza kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu,” alisema.

Alisema ni matarajio yao majadiliano yatafanyika kwa kuheshimiana, kutumia hoja za kizalendo na kiungwana na kuangalia kwa mapana mambo na masuala makuu yaliyopendekezwa katika rasimu hiyo.

Idadi ya Serikali

Alipoulizwa msimamo wake ni nini kuhusu muundo wa serikali, Askofu Ngalalekumtwa alisema “siwezi kusema popote pale, naogopa kuwapa ushawishi watu wetu na ndio maana msimamo wa Kanisa ni kuwataka wajumbe wote warejee, wajadiliane na kutuletea Katiba itakayokuwa na sifa hizo.”

Hata hivyo muundo huo wa Serikali, ndio uliogeuka kiini cha mjadala wa Katiba mpya kuliko suala lingine, ambapo baadhi ya wajumbe hasa wa vyama vya Upinzani, waliunda kundi lao walilojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakitetea serikali tatu, yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.

Kuundwa kwa kundi hilo, kulichangia kuibuka kwa kundi la Tanzania Kwanza, ambalo linaundwa na wajumbe wengi kutoka CCM ambalo linatetea muundo wa serikali mbili, yaani Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, likiamini kuwa serikali tatu zitaivunja Tanzania na kuleta machafuko.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency