Home » » Daktari Yanga avujisha siri za wachezaji.

Daktari Yanga avujisha siri za wachezaji.

ALIYEKUWA Daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya, amesema wapo wachezaji wengi nchini wenye majeraha makubwa kuliko yale yaliyokuwa yakimkabili kiungo wa Azam, Frank Domayo ila klabu zao zimeshindwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuwahudumia.
Domayo alifanyiwa operesheni ya nyama za paja wiki iliyopita na atakaa nje ya uwanja hadi Januari mwakani. Kiungo huyo wa zamani wa Yanga aliumia miaka miwili iliyopita lakini alikuwa akificha majeraha hayo kwa kuhofia kupoteza namba Yanga.
Matuzya alisema: “Klabu zetu zinaangalia zinapata nini kwa mchezaji na si maisha ya wachezaji, Yanga walilifahamu tatizo la Domayo lakini walilichukulia poa, vivyo hivyo timu nyingine nazo zinavyofanya kwa wachezaji wao, ni imani yangu kuwa wapo wengi wenye maumivu makali zaidi ya hayo lakini wanaogopa kusema.
“Nawapongeza Azam kwa kuwa na utaratibu mzuri, wanajali wachezaji wao na wamewahakikishia ajira zao hata kama watakuwa majeruhi, huu ni mfano wa kuigwa na timu kongwe za Simba na Yanga,” alisema Matuzya
Kauli hiyo ya Matuzya inaendana na kauli ya Dokta Gilbert Kigadye ambaye aliwahi kukaririwa na Mwanaspoti akisema kuwa wapo baadhi ya wachezaji nchini aliowapa ushauri wa kukaa nje ya uwanja kwa miezi sita au zaidi lakini walikaidi maelekezo hayo kwa hofu ya kupoteza namba katika timu zao na amekuwa akiwashuhudia wakicheza wakiwa wagonjwa.
Kigadye ni mtaalamu wa mifupa ambaye amekuwa akiwatibu wachezaji wengi nchini lakini alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la wachezaji kuficha majeraha yao.
Share this article :
 
Copyright © March 2012. MARIDADI AGENCY
-Haki zote zimehifadhiwa
- All Rights Reserved
Template Modified by Hassan Moh Toziri
Published by Maridadi Agency